TUNA JUKUMU LA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI – DKT. NYAKIROTO
Posted on: November 13th, 2025Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dkt. Museleta Nyakiroto, amewasihi watumishi wa hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma bora, zenye upendo na weledi kwa wananchi wanaofika kupata matibabu.
Akizungumza katika Kikao cha Watumishi Wote kilichofanyika hospitalini hapo, Dkt. Nyakiroto alisema utoaji wa huduma bora ni wajibu wa kila mtumishi wa afya, kwani wananchi wanaowafikia wanategemea huduma zenye ubora na huruma.
"Tunalo jukumu la kuhakikisha kila mwananchi anayefika hospitali yetu anapata huduma nzuri. Hii ndiyo dhamira yetu kama watumishi wa umma,” alisema Dkt. Nyakiroto.
Katika kikao hicho, watumishi walipata fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu kuboresha huduma na kuongeza mapato ya hospitali, sambamba na kukumbushana miongozo na maadili ya utumishi wa umma.
Kupitia kikao hicho watumishi walipata nafasi ya kuwasilisha changamoto zao za kikazi, ambapo menejimenti ya hospitali iliahidi kuzifanyia kazi kwa wakati ili kuimarisha mazingira bora ya utoaji huduma.
Aidha, Dkt. Nyakiroto alihitimisha kwa kuwataka watumishi wote kuendelea kushirikiana, kuwa na nidhamu, na kuzingatia misingi ya maadili ya kazi, akisisitiza kuwa mafanikio ya hospitali yanategemea umoja na utendaji wa pamoja.





