Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

WAJUMBE WA BODI YA USHAURI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA WAENDELEA KUWEKA MIKAKATI YA UBORESHAJI WA HUDUMA BRRH

Posted on: November 26th, 2025

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba wameendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma baada ya kufanya kikao chao leo na kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya hospitali hiyo.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. George Buberwa, kilihusisha mapokezi ya taarifa mbalimbali kutoka kwa wakuu wa idara na vitengo, zikiwemo changamoto na mafanikio ya kiutendaji kutoka kwa wakuu wa idara na vitengo ambayo yanahitaji kupatiwa ufumbuzi.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Buberwa alisema kuwa wajibu mmojawapo wa bodi ni kupokea na kuchambua changamoto za kiutendaji na utoaji wa huduma na kuzifanyia kazi ili kuboresha mazingira ya utoaji huduma.

“Sisi kama Bodi ya Ushauri tunahakikisha changamoto zote za kiutendaji zinajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi ili hospitali yetu iendelee kutoa huduma bora na salama kwa wananchi,” alisema.

Aidha, Dkt. Buberwa alisisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma kwa wateja (wagonjwa) na kuwataka watumishi wa hospitali kuzingatia misingi ya maadili, uadilifu na heshima katika kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba, Dkt. Museleta Nyakiroto, aliishukuru Bodi kwa ushauri na ushirikiano wao akisema kuwa mapendekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi ili kuendelea kuinua kiwango cha utoaji huduma.

“Tunawashukuru sana kwa mwongozo na ushirikiano wenu, yote mliyoshauri tumeyapokea na tutaendelea kuyafanyia kazi kwa ufanisi,” alisema Dkt. Nyakiroto.

Kikao hicho kinaendelea kuonesha dhamira ya pamoja kati ya uongozi wa hospitali na Bodi ya Ushauri katika kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Kagera wanapata huduma stahiki.