WATAALAM WA FIZIOTHERAPIA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA WAELEZA UMUHIMU WA HUDUMA ZA FIZIOTHERAPIA HUSUSANI MAZOEZI TIBA KWA WATOTO WENYE MATATIZO YA MAUNGIO
Posted on: February 12th, 2026Wataalam wa Fiziotherapia (Physiotherapy) kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba wameeleza umuhimu wa huduma wanazotoa mojawapo ikiwa ni mazoezi tiba kwa watoto wenye matatizo ya maungio, wakibainisha kuwa huduma hiyo ina mchango mkubwa katika kurejesha afya, uwezo wa viungo na kuboresha maisha ya watoto hao.
Elimu hiyo imetolewa leo wakati wa kikao cha elimu endelevu kazini (CME) kilichowakutanisha watumishi wote wa hospitali hiyo, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu namna ya kutambua mapema matatizo ya maungio kwa watoto na umuhimu wa kuwapeleka hospitalini kwa wakati.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Fiziotherapia wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba, Dismas Melichory, amesema kuwa watoto wenye matatizo ya maungio huonesha dalili mbalimbali zikiwemo kushindwa kutumia vizuri viungo kama mikono au miguu, kushindwa kusimama au kutembea, maumivu ya mara kwa mara kwenye viungo, pamoja na maungio kuwa magumu au kupinda isivyo kawaida.
Amefafanua kuwa huduma ya mazoezi tiba husaidia kuimarisha misuli, kurekebisha mkao wa mwili, kupunguza maumivu na kuongeza uwezo wa mtoto kufanya shughuli za kila siku kulingana na umri wake.
Aidha, amesema kuwa matibabu hayo yanahitaji ufuatiliaji wa karibu na ushirikiano kati ya wataalam wa afya na wazazi au walezi.
Afisa Fiziotherapia Dismas amesisitiza kuwa matatizo mengi ya maungio kwa watoto yanatibika, hususan pale mtoto anapowahishwa hospitalini mapema kwa ajili ya uchunguzi na kuanza matibabu.
Ameongeza kuwa kuchelewa kuwapeleka watoto hospitalini kunaweza kusababisha hali kuwa ngumu zaidi na kuathiri ukuaji na maendeleo yao ikiwa ni pamoja na kushindwa kushuriki katika shughuli mbali mbali mfano shughuli binafsi au shughuliza kijamii





