Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

WATUMISHI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA WAJENGEWA UWEZO KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA DHARURA

Posted on: February 20th, 2026

Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba wamepatiwa mafunzo maalum ya utoaji wa huduma za dharura na mahututi (Emergency and Critical Care Capacity Building), yakilenga kuimarisha utoaji wa huduma za haraka, salama na zenye ubora kwa wagonjwa walioko katika hali hiyo.

Mafunzo hayo yametolewa na Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Kanda Bugando, yakihusisha elimu ya nadharia na vitendo kwa lengo la kuwajengea watumishi ujuzi wa kisasa katika utambuzi wa haraka wa hali za dharura, uokoaji wa maisha pamoja na ufuatiliaji wa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Dkt. Debora Madyedye Dakatari Bingwa wa Usingizi na Ganzi Salama Kutoka Hospitalia ya Kanda Bugando alisema kuwa, mafunzo yamelenga kuongeza uwezo wa watumishi na kubadilishana ujuzi katika kushughulikia wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura na uingiliaji wa haraka wa kitabibu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba baada ya mafunzo kutamatika Dkt Sophia Mosha ambaye pia ni Dakatari Bingwa wa Watoto amewashukuru wakufunzi kwa elimu waliyoitoa huku akiwaomba watumishi wote walipatiwa elimu hiyo kuitumia vyema katika utoaji wa huduma.