WATUMISHI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA WAPATIWA ELIMU KUHUSU HAKI NA WAJIBU WA MTEJA NA MTOA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: November 27th, 2025Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba wamepatiwa elimu muhimu kuhusu Haki na Wajibu wa Mteja (mgonjwa) na Mtoa Huduma za Afya kupitia wasilisho lililotolewa na Afisa Tawala na Rasilimali Watu wa hospitali hiyo, Simon Njeya katika kikao cha CME.
Katika wasilisho hilo, ameeleza kwa kina umuhimu wa wahudumu kuwahudumia wagonjwa kwa kufuata misingi ya heshima, maadili, faragha na usalama wa mgonjwa, sambamba na kutoa huduma bora bila ubaguzi.
Amefafanua pia kuwa mgonjwa ana haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu afya yake, kushiriki maamuzi ya matibabu, na kulindwa taarifa zake binafsi. "Mginjwa anapofika katika kituo cha kutolea huduma anakuwa na haki ya kupata huduma bora bila ubaguzi, haki ya kuheshimiwa na kutunzwa utu wake, haki ya kupata taarifa sahihi na kwa lugha inayoeleweka, haki ya usiri wa taarifa zake, haki ya kukataa au kukubali matibabu, haki ya kupata rekodi za matibabu yake, haki ya huduma za dharura bila vikwazo na haki ya kutoa malalamiko bila kuonewa au kulipiziwa kisasi."
Pia amekumbusha kuwa ni wajibu wa mteja kutoa taarifa za kweli kuhusu afya yake, kufuata maelekezo ya matibabu, na kuheshimu taratibu za hospitali.
Aidha, mtoa huduma wa afya naye ana haki zake za msingi ambazo zinapaswa kulindwa, ikiwemo haki ya kufanya kazi katika mazingira salama bila vitisho au unyanyasaji, haki ya kuheshimiwa na kulindwa kisheria anapotekeleza majukumu yake, haki ya kupata taarifa sahihi kutoka kwa mgonjwa ili kutoa huduma bora, haki ya kupatiwa vifaa na rasilimali muhimu, haki ya kupumzika kulingana na utaratibu wa kazi, na haki ya kupata mafunzo endelevu (CME) ili kuboresha ujuzi na uwezo wake katika utoaji wa huduma bora.





