WATUMISHI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA WAPATIWA ELIMU YA MATIBABU YA NJANO KWA WATOTO WACHANGA
Posted on: January 23rd, 2026Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba wamepatiwa elimu maalum ya jinsi ya kuwahudumia watoto wachanga wanaokabiliwa na ugonjwa wa manjano, unaojulikana kitaalamu kama Neonatal Hyperbilirubinemia, kupitia mafunzo ya elimu endelevu ya tiba (CME).
Elimu hiyo imetolewa na wataalamu wa afya kutoka Idara ya Watoto ya hospitali hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa watoto wachanga, kwa lengo la kubaini ugonjwa huo mapema na kutoa matibabu sahihi kabla haujaleta madhara makubwa.
Akitoa mada kuhusu ugonjwa huo, Daktari Enock Doli amesema kuwa manjano kwa watoto wachanga husababishwa na kuongezeka kwa kiwango cha bilirubini kwenye damu, hali inayotokana na ini la mtoto mchanga kutokuwa limekomaa vya kutosha kuchakata bilirubini hiyo.
Ameeleza kuwa sababu nyingine zinazosababisha ugonjwa huo ni pamoja na kuvunjika kwa kasi kwa chembechembe nyekundu za damu, kutokulingana kwa damu kati ya mama na mtoto (ABO au Rh incompatibility), maambukizi, kuzaliwa kabla ya wakati, pamoja na mtoto kutonyonya vizuri katika siku za mwanzo baada ya kuzaliwa.
Dkt. Doli ameongeza kuwa iwapo ugonjwa wa manjano hautagundulika na kutibiwa mapema, unaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtoto, ikiwemo uharibifu wa ubongo (kernicterus), kupoteza uwezo wa kusikia, mtoto kuwa mlegevu au kushindwa kunyonya, kulia kwa sauti isiyo ya kawaida, na katika hali kali zaidi kusababisha ulemavu wa kudumu au kifo.
Amesisitiza umuhimu wa wahudumu wa afya kuwa makini katika ufuatiliaji wa hali ya watoto wachanga, hasa ndani ya siku chache za mwanzo baada ya kuzaliwa, na kuhakikisha wanapatiwa matibabu sahihi ikiwemo tiba ya mwanga (phototherapy) kulingana na hali ya mtoto.
Aidha, amewahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto hospitalini mapema wanapoona dalili za manjano, badala ya kutumia imani potofu au tiba zisizo rasmi, akibainisha kuwa ugonjwa wa manjano kwa watoto wachanga unatibika iwapo utagundulika mapema na kutolewa huduma stahiki 





