Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

BUKOBA RRH YASHIRIKI SABASABA KWAKUTOA HUDUMA ZA VIPIMO, ELIMU NA USHAURI WA AFYA BURE KWA WANANCHI.

Posted on: July 4th, 2024

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba (Bukoba_RRH) imeshiriki maonyesho ya Biashara, Viwanda, Utalii na Bidhaa za Kilimo yanayoendelea katika viwanja vya CCM Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera kwa kutoa huduma ya vipimo, Elimu na Ushauri wa Afya bure kwa wananchi wote wanaotembelea banda lao.

Akitoa maelekezo na ukaribisho kwa wananchi waliofika katika banda la kutolea huduma la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Afisa Habari na Uhusiano wa hospitali hiyo, Titus Mwombeki amesema kuwa huduma za zinazotolewa bure katika banda lao ni pamoja na huduma ya upimaji wa Sukari, Virusi vya UKIMWI, Huduma ya Elimu na Ushauri wa Lishe pamoja na Uchangiaji wa Damu kwa wananchi wanaowiwa kuchangia.

"Tunaendelea kuwakaribisha wananchi wote wanofika katika viwanjai vya sabasaba waweze kutembelea banda letu la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba ili waweze kupima afya zao bure, sisi kama hospitali mama ya mkoa tunatoa huduma ya vipimo bure ikiwa ni pamoja na kupima sukari, UKIMWI utoaji wa elimu ya Jinsia na Ukatili kwa watoto, Elimu juu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na Uchangiaji wa damu" amesema Mwombeki.

Sambamba na hilo amewasihi wananchi kuendelea kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba ili waweze kukutana na Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho, Magonjwa ya akina Mama, Upasuaji, Daktari Bingwa wa Sikio, Pua na Koo, Uzazi na Kizazi, Daktari Bingwa wa Watoto pamoja na Wataalam wa Lishe.