Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

RAS APONGEZA UTENDAJI KAZI WA WATUMISHI WA AFYA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA.

Posted on: October 7th, 2023


Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Toba Nguvila ameipongeza menejimenti  ya Hospiatali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba hususani Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo pamoja na watumishi wote kwa kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.

Aliyasema hayo Octoba, 6 mwaka huu alipotembelea Hospiatali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba (BRRH) na kuongea na watumishi wa hospitali hiyo juu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi na utendaji kazi.

“Nachukua nafasi hii kuwapongeza watumishi wote wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba hususani Mganga  Mfawidhi wa hospitali hii kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya ya kunusuru maisha ya Watanzania, binafsi nimekuja mara nyingi katika Hospitali hii kupata huduma lakini nimekuwa nikipokelewa vizuri na majibu ya vipimo yanatoka kwa wakati, hongereni sana”

Katibu Tawala, alisema kuwa kwa sasa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba inaendelea kukua na kupanuka katika suala zima la utoaji wa huduma baada serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya kuleta madaktari bingwa, vifaa vya kisasa pamoja na uboreshaji wa miundombinu katika hospitali hii.

“Huduma katika Hospitali hii zimeboreshwa sana, kwasasa tumepata madaktari bingwa ambao kipindi cha nyuma hatukuwa nao, kuna vifaa vipya navya kisasa vinavyotumika kupima magonjwa mbalimbali mfano mashine ya CT-SCAN , vifaa vya kisasa vya upasuaji na vinginevyo, lakini pia tunaona majengo yanazidi kujenjwa na hivi punde yataanza kutumika mfano jengo la kisasa la ICU na Emergency Medical Department (EMD)”

Sambamba na hilo, amewasihi watumishi wa BRRH kuendelea kufanya kazi zao kwa weledi kwa kuzingatia maadili ya kazi yao pamoja na miongozo iliyowekwa na Wizara ya Afya kama ambavyo mamekuwa wakifanya kila siku ili wananchi waendelee kufurahia huduma zinazotelewa hospitalini hapo huku akisema kuwa changamoto zilizowasilishwa na watumishi hao zitafanyiwa kazi.