Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

UWEPO WA MASHINE YA KISASA YA CT-SCAN HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA YABORESHA HUDUMA

Posted on: January 26th, 2025

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, ameeleza kufurahishwa na uwepo wa mashine ya kisasa ya CT-Scan katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera ambayo imewawezesha Madaktari katika hospitali hiyo kuanza kutoa huduma za upasuaji wa awali wa ubongo kwa wagonjwa wa dharura.

Dkt. Magembe ametoa kauli hiyo leo Januari 26, 2025 alipotembelea hospitali hiyo kwa ziara maalum yenye lengo la kukagua utoaji wa huduma za afya hospitalini hapo na kujionea jinsi watumishi wanavyoendelea kuchukua tahadhari katika kujikinga na magonjwa wakiwa kazini.

“Nimefurahishwa sana na jinsi mashine ya CT-Scan inavyosaidia madaktari wetu kutoa huduma za upasuaji wa awali wa ubongo kwa wagonjwa wa dharura hasa waliopata ajali na kuvuja na damu kichwani, kwani kwa sasa wagonjwa hao wanapata huduma hapa kitu ambacho sio cha kawaida kwa hospitali ya Mkoa kutoa huduma hii, mara nyingi huduma kama hii utolewa na hospitali za Kanda au Taifa,” amesema Dkt. Magembe.

Akiwa katika ziara hiyo, Dkt. Magembe pia ametembelea Kitengo cha Watoto Wachanga (NCU) na kupongeza watumishi wa kitengo hicho kwa kuendelea kutoa huduma bora, kujituma na kufuata miongozo ya kitaalam ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Aidha, ametembelea Jengo la Dharura (EMD) na Kitengo cha Kusafisha Damu (Dialysis) ambapo aliwapongeza watumishi kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora kwa lengo la kuokoa maisha ya Watanzania.

Dkt. Magembe amesisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za afya nchini kwa kusambaza vifaa tiba vya kisasa, kujenga hospitali mpya za wilaya, na kuanzisha vituo vya afya ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dkt. Museleta Nyakiroto amemshukuru Dkt. Magembe kwa kutembelea hospitali hiyo na kuahidi kuwa wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba wataendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kufuata miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya.