Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

WANANCHI WASHAURIWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA ZAO KABLA YA KUINGIA KWENYE NDOA KUKATA MNYORORO WA KUSAMBAA KWA UGONJWA WA SELIMUNDU.

Posted on: September 27th, 2023


WANANCHI wameshauriwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao  kabla ya kuingia kwenye ndoa  ili kuweza kukata mnyororo wa uwepo wa  ugonjwa wa selimundu (Sickle Cell Desease) kwani itapelekea kuokoa maisha yao na watoto wao 

Nasaha hiyo imetolewa na wataalamu wa Afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Bukoba (BRRH) walipotembelea shule ya  sekondari Rugambwa, Kaizilege, na  Ihungo zinazopatikana Mnispaa ya Bukoba Mkoani Kagera na kutoa elimu kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ikiwa ni mwendelezo wa utoaji  elimu kwa jamii juu ya ugonjwa wa selimundu (Sicle Cell Disease).

Akitoa elimu hiyo, Dkt. Sophia Mosha , amesema kuwa mwezi Septemba kila mwaka ni mwezi wa uelimishaji wa jamii juu ya ugonjwa wa selimbundu, hivyo Hospitali ya Rufaa Mkoa, Bukoba kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wanaungana na Dunia nzima  kuadhimisha mwezi huu kwa kutoa elimu, ushauri na upimaji wa awali wa ugonjwa  wa selimundu kwa watoto pamoja na watu wazima wakiwemo wanaotarajia kufunga ndoa ikiwa ni njia moja wapo ya kupambana na ugonjwa huo.

“Ugonjwa wa  Selimundu ni ugonjwa wa kurithi, unarithiwa kutoka kwa baba na mama wote wawili nasio kwa mzazi mmoja tu, hivyo kupima afya  kabla ya kuingia kwenye ndoa ni suala muhimu kwani husaidia wananchi kujijua kama wana vinasaba vya selimundu wote kwa pamoja au hawana, kwahiyo tunaposhauri wananchi kupima kabla ya kuanzisha familia lengo ni wasiende kuwa na wenza ambao wote (mme na mke) wana vinasaba vya ugonjwa wa selimundu, mkipima mapema na kuhakikisha hamna vinasaba au mmoja anavyo mwingine hana mnapata uwakika wa  mtoto atakayepatikana atakuwa hana ugonjwa huo, hapa tutakuwa tumekata mnyororo”

Ameongeza kuwa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba mwezi huu , wanatoa huduma ya upimaji wa awali kwa watoto wote wanaozaliwa katika hospitali hiyo na ikibainika mtoto ana ugonjwa huo anaanzishiwa klini na atafuatiliwa ili aweze kusaidiwa kwa kuzingatia miongozo iliyowekwa na Wizara ya Afya na baada ya mwezi huu huduma ya upimaji kwa lika zote itaendelea kutolewa kama kawaida kwa kuchangia kiasi kidogo lengo likiwa ni kupambana na ugonjwa huu.

Kwa upande wake, Dkt. Immaculate Kalungi alisema kuwa, dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mtu kuishiwa damu mara kwa mara, kuwa na macho ya njano, kuvimba paji la uso, kuugua mara kwa mara pamoja na ukuaji hafifu kwa upande mtoto.

Kwa upande wake,  Private Selestine ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita (PCM)  shule ya sekondari Ihungo , amewapongeza wataalamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba kwa kuwatembelea na kuwapatia elimu juu ya ugonjwa huo, huku akisema kuwa wao kama vijana watakuwa mabalozi wa kwa jamii zao ili waone umuhimu wa kupima afya kabla ya kuingia kwenye ndoa huku akisisitiza kuwa nao watazingatia ushauri huo pindi watakapo fikia hatua ya kuwa na familia zao baada ya kumaliza masomo yao.