Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

JOPO LA MADAKTARI BINGWA BUKOBA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA WAFANIKIWA KUTOA PUNJE YA MUHINDI KWA MTOTO MWENYE UMRI WA MIAKA NNE (4) ILIYOKWAMA KWENYE NJIA YA HEWA

Posted on: January 20th, 2025

Madaktari Bingwa wa Sikio, Pua na Koo (ENT) wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Kagera kwa kushirikiana na timu ya wataalamu wa usingizi wamefanikiwa kumuokoa mtoto wa miaka minne (4) aliyekuwa na punje ya mahindi iliyokwama kwenye njia ya hewa.

Daktari Bingwa wa Sikio, Pua na Koo, Dkt. Richard Shija, alisema kuwa mtoto huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa na matatizo makubwa ya kupumua, hali iliyosababisha timu ya madaktari kufanya uchunguzi wa haraka ili kunusuru uhai wa mtoto huyo.

“Baada ya uchunguzi, tulibaini kuwa kulikuwa na punje ya mahindi iliyokwama katika njia ya kuelekea pafu la kushoto (left bronchus). Tukampeleka chumba cha upasuaji na kufanikisha kutoa punje hiyo kwa kutumia kifaa maalum kiitwacho 'bronchoscopy'' alisema Dkt. Shija.

Aliongeza kuwa hudama hiyo ilitolewa kwa ushirikiano wa karibu kati ya timu ya ENT na wataalamu wa usingizi, na kwamba zoezi hilo lilimalizika kwa mafanikio makubwa, Kwa sasa mtoto huyo anaendelea vizuri baada ya matibabu.