Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

MSD MAKAO MAKUU NA KANDA WATEMBELEA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA, MAADHIMIO YA MIAKA 30 YA TAASISI HIYO

Posted on: January 5th, 2025

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba leo tarehe 6 Januari 2025, imepokea ugeni wa Maafisa wa Bohari ya Dawa (MSD) kutoka makao makuu wakishirikiana na MSD Kanda.

Ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo muhimu katika sekta ya afya nchini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bi. Rosemary Silaa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD alisema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kukagua ubora wa bidhaa zinazotolewa na MSD, hali ya upatikanaji wa dawa na vitendanishi katika hospitali hiyo, pamoja na kufuatilia changamoto zozote zinazoweza kujitokeza katika utoaji wa huduma hizo.

"Ziara hizi ni sehemu ya juhudi za MSD kuhakikisha kuwa tunaboresha zaidi huduma tunazotoa na kuendelea kujifunza mahitaji ya wateja wetu ili kutoa huduma bora"

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba, Dkt. Sophia Mosha, aliwashukuru MSD kwa huduma bora wanazotoa ambazo zimechangia kuboresha afya za wananchi wa Kagera. Pia aliwaomba viongozi wa MSD waendelee kutembelea hospitali hiyo mara kwa mara ili kujionea hali halisi na kuimarisha ushirikiano.

"Tunawashukuru sana MSD kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha hospitali yetu inapata dawa na vifaa muhimu. Tunawasihi muendelee na moyo huu wa kutembelea vituo vyetu vya afya mara kwa mara," alisema Dkt. Mosha.

Ziara hiyo ilihitimishwa kwa mazungumzo baina ya maafisa wa MSD na viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba huku wakikubaliana kushirikiana kwa karibu zaidi katika kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera.