Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

SERIKALI KUJENGA JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA

Posted on: January 3rd, 2025

Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga kujenga jengo maalum la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Bukoba, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuboresha huduma za afya nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo, Januari 3, 2025 na Waziri wa Afya, Mheshimiwa Jenesta Mhagama katika hafla ya ugawaji wa Vifaa kwa Maafisa wa Afya ngazi ya jamii iliyofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Mkoani Kagera.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya juhudi kubwa ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kujenga Vituo vya Afya, Zahanati, Hospitali za Wilaya nchini na kuhakikisha hospitali hizo zinakuwa vifaa vya kisasa pamoja na dawa zakutosha.

"Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za afya nchini zinapatikana kwa urahisi nchi nzima, kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, tumeamua tutajenga jengo maalum la Mama na Mtoto ili kuhakikisha huduma za mama na mtoto zinapatikana na kutolewa kihurahisi katika hospitali hii"

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajat Fatma Mwassa, amemshukuru Waziri wa Afya na serikali kwa ujumla kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuboresha sekta ya afya huku akisisitiza kuwa hali ya utoaji wa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba inaridhishwa.

"Tunaishukuru Serikali yetu kwa kujenga vituo vya afya, zahanati na hospitali za Wilaya hapa mkoani Kagera, kiukweli Huduma zinazotolewa katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba niza kiwango cha juu, hata mimi binafsi nikiumwa huwa napata huduma hapa siendi tena nje" alisema Hajat Mwassa.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dr. Samwel Laizer amemshukuru mheshimiwa Waziri wa Afya kwa kuutembelea Mkoa wa Kagera huku akisema kuwa wao kama viongozi wataendelea kuwasimamia watumishi wa Afya katika Mkoa wa Kagera kuahakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi kwa kufuata miongozo inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya