TIMU YA DHARURA YA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, BUKOBA YAENDELEA KUWEKA MIKAKATI YA KUPAMBANA NA UGONJWA WA KIPINDUPINDU.
Posted on: January 8th, 2024Timu ya Dharura ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba (BRRH-RRT) imekaa kikao cha dharula na kupeana mipango na mikakati mbalimbali jinsi ya kuendelea kukabiliana na magonjwa ya mlipuko hususani ugonjwa wa kipindupindu.
Kikao hicho, kimefanyika leo Januari 09, 2024 katika ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (ukumbi wa Darasa) kikiongozwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Dkt. Museleta Nyakiroto.
Kupitia kikao hicho, kila mjumbe wa BRRH-RRT amekumbushwa majukumu na wajibu wake kulingana na nafasi yake anayohudumu katika kukabiliana na matukio ya dharula yanapotokea huku wakielezwa mikakati na hatua za haraka ambazo zimeishachukuliwa na menejimenti ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba katika kukabiliana na magonjwa wa kipindupindu.
“Kila mjumbe wa anayeunda Timu ya Dharura ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba (BRRH-RRT) anaowajibu wa kushiriki kikamilifu linapotokea jambo la dharula katika eneo letu la kazi, hivyo tunapaswa kukaa chonjo na tunatakiwa kutokea mara moja pindi anapohitajika”
Aidha, kutokana na uwepo wa kipindupindu Mkoani Kagera Menejimenti ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba imechukua hatua mbalimbali za kuwalinda na kuwakinga na ugonjwa wa kipindupindu wananchi wanaofika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba kupata huduma ya matibabu, ushauri wa Afya na kuwaona ndugu zao waliolazwa hapa Hospitalini.
Hatua hizo ni pamoja na kutenga sehemu mahususi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wanaobainika kuwa na ugonjwa wa kipindupindu baada ya kufika hapa BRRH, kuwahimiza wananchi waofika hapa BRRH kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kila wafikapo lango la kuingilia Hospitalini na wakati wa kutoka (getini), kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kabla na baada ya kutoka wodini kuwaona ndugu zao waliolazwa , kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono pamoja na na kuepuka kula chakula baridi uwapo maeneo ya Hospitali.
Sambamba na hilo timu hiyo na wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba wamesisitizwa kuendelea kuzingatia miongozo yote ya Afya ikiwemo miongozo ya ya kuzuia Maambukizi sehemu zao za kazi (IPC).