WANANCHI KAGERA WATAKIWA KUFIKA VITUO VYA AFYA WANAPOHISI DALILI ZISIZO ZA KAWAIDA
Posted on: January 23rd, 2025Wananchi wametakiwa mkoani Kagera wamatakiwa kufika katika kituo cha afya mapema pale wanapohisi kuwa dalili zalisizokuwa za kawaida.
Rai hiyo imetolewa leo Januari 24, 2025 na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe alipowasili wilaya ya Biharamulo mkoani humo kujionea na akikagua hatua za kudhibiti ugonjwa wa Marburg katika wilaya hiyo na kuwataka wakazi wa wilaya hiyo kuendelea na shughuli zao za kijamii huku wakiendelea kuchukua tahadhari.
"Tuna mazoea ya kujitibu nyumbani, kwa kutumia miti shamba, kujifukiza, au kutumia dawa za kupunguza maumivu kama 'paracetamol' bila kufahamu chanzo cha ugonjwa. Ucheleweshaji huu mara nyingi unaleta madhara makubwa, kwani unasababisha watu kugundulika na maambukizi tayari muda umeshakwenda," amesema Dkt. Magembe.
Amewaomba wananchi kuwahi vituo vya afya mara tu wanapoona dalili zisizo za kawaida ili vipimo na matibabu yafanyike mapema.
Aidha, Dkt. Magembe amehimiza wananchi kubadilisha baadhi ya tabia za kijamii ambazo zinaweza kusababisha maambukizi zaidi, kama kushikana mikono au kukumbatiana wakati wa kusalimiana.
Sambambana hilo, Dkt. Magembe amesisitiza kuwa, Serikali imejipanga kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, mashuleni na maeneo yenye mikusanyiko ya watu.
"Elimu kwa umma ni msingi wa mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Tutaendelea kufikisha ujumbe sahihi kwa wananchi wote popote walipo," amesisitiza.
Ameongeza kuwa katika juhudi za kudhibiti ugonjwa wa Marburg, Serikali imeweka wataalamu wa afya katika maeneo yote ya mipaka ya nchi ili kuhakikisha wageni wote wanaoingia nchini wanakaguliwa afya zao.
"Wakitakiwa kuwapimwa joto au kuulizwa maswali, tuchukulie hatua hiyo ni kwa nia njema ya kuhakikisha tunaudhibiti ugonjwa huu," amesema Dkt. Magembe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt.Ntuli Kapologwe amesema kuwa mbali na mgonjwa mmoja aliyepo, Serikali imewaweka karantini wahisiwa 15 nawengine 281 waliochangamana na wahisiwa hao, mpaka sasa watu wawili wamefariki kutokana na ugonjwa huo.