Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba
(Government Hospital)

WATUMISHI WA AFYA BRRH WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO MPYA WA PEPMIS

Posted on: January 20th, 2024

Watumishi wa Afya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba wamepatiwa mafunzo ya siku mbili ya mfumo mpya wa Public Employees Performance Management Information System (PEPMIS) unaolenga kupima utendaji kazi kwa kila mtumishi wa Umma.

Mafunzo hayo yalitolewa Januari 18, 2024 hadi Januari 19, 2024 katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Maafisa kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambao ni Jeanfrida Byera Mushumbusi na Esther Samwel Komba.

Akitoa Mafunzo hayo Esther Samwel Komba alisema kuwa, mfumo wa PEPMIS ni mfumo mpya  na mbadala wa mfumo wa OPRAS, utakaosaidia mtumishi mmoja mmoja wa umma  kutimiza kajukumu yake ipasavyo  kwa kutumia mtandao.

“Huu ni mfumo mzuri unaolenga kupima utendajikazi wa kila siku wa mtumishi wa Umma, hivyo mfumo huu utasaidia sana watumishi wa umma kutimiza majukumu yao kwa ufasaha na kwa wakati”

Akitoa neno la shukrani Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Dkt. Museleta Nyakiroto aliwashukru wawezeshaji wa mafunzo ya mfumo wa PEPMIS kwa darasa zuri huku akiwasihi watumishi walioshiriki mafunzo hayo kuyatilia maanani yote waliofundishwa na wakufunzi hao kwani yatawasaidia pindi watakapoanza kutumia mfumo huo.